2 Juni 2024 - 15:32
Maandamano ya kutaka kusitishwa 'jinai za kivita' Gaza yaendelea kufanyika Ulaya na Asia

Maandamano ya kulaani mauaji ya halaiki yanayofanywa na jeshi la uutawala haramu wa Israel huko Gaza yanaendelea kushuuhudiwa katika mataifa mbalimbali barani Ulaya na Asia.

Mataifa kadhaa ya Ulaya na Asia yameendelea kushuhudia maandamano makubwa kwa siku kadhaa mtawalia ya kutaka kusitishwa mara moja uvamizi na jinai za Israel huko Gaza na na kuruhusu kuingia misaada ya kibinadamu.

Mji mkuu wa Denmark, Copenhagen, umeshuhudia maandamano makubwa, ambapo waandamanaji walizunguka katika mitaa mingi, wakiimba nara za kutaka kusitishwa mara moja kwa jinai hizo na kutoa mwito wa kushtakiwa viongozi wa utawala huo ghasibu wakiwataja kuwa wahalifu wa kivita. Maandamano kama hayo yameshuhudiwa katika mji mkuu wa Ujerumani Berlin ambapo waandamanaji wameitaka serikali yao kuusitisha ushirikiano na Israel huku wakiitaka pia jamii ya kimataifa kuwaunga mkono wananchi wa Palestina. 

Wakati huo huo, mji mkuu wa Ufaransa Paris nao umeendelea kushuhudia maandamano ya kulaani jinai za Israel na kutangaza kuwaunga mkono wananchi wa Palestina hususan  wa Gaza wanaokabiliwa na hujuma na mashambulio ya kinyama ya Israel.

Barani Asia nchi za Indonesia na Pakistan nazo zimeshuhudia maandamano makubwa ya kuunga mkono Palestina na kulaani jinai zinazofanywa na utawala haramu wa Israel huko Gaza.

Waandamanaji hao wameonyesha kuchukizwa kwao mno na jinai za Israel dhidi ya wanawake na watoto watoto wadogo wasio na hatia wa Palestina na kuonyesha mshangao wao kwa uzembe wa Umoja wa Mataifa na baraza lake la usalama katika kushughulikia maafa ya Gaza.

342/